Back to top

Miili 94 ya watu waliozama ziwa Victoria yaopolewa.

21 September 2018
Share


Zoezi la uokoaji na uopoaji wa miili ya watu waliokuwa kwenye kivuko cha MV.Nyerere kilichopinduka na kuzama kikitoka Bugorora kwenda kisiwa cha Ukara katika ziwa Victoria linaendelea ambapo hadi sasa miili 94 imeopolewa na waliookolewa wakiwa hai wanazidi 40.

Vikosi vya uokoaji mkoa wa Mwanza vimeongezewa nguvu na vikosi vya mkoa wa Mara katika eneo la tukio kuongeza kasi ya kuokoa na kuopoa watu waliopinduka na kivuko hicho.

Mkuu wa Jeshi la polisi IGP Simon Sirro na Waziri wa Uchukuzi Isaac Kamwelwe wamefika eneo la tukio kushiriki uokoaji.

Wakati uokoaji na uopoaji ukiendele mamia ya wakazi wa visiwa hivyo wamefurika kituo cha afya cha Bwisya kutambua jamaa zao walioopolewa.

Tayari uongozi wa wakala wa meli mkoa wa Mwanza umetambua wafanyakazi wa kivuko watano ambao wamepoteza maisha akiwemo   nahodha, fundi, Karani, mlinzi na mkuu wa kivuko, Kivuko hicho kilikuwa na wafanyakazi wanane.

Mwandishi wetu aliyeko eneo la tukio amesema wengi walioopolewa hadi sasa ni wanawake.