Back to top

Miili ya wahabeshi 8 yatelekezwa hospitali ya Bombo kwa miezi miwili.

15 January 2019
Share

Idara ya uhamiaji mkoani Tanga imeziomba mamlaka za kimataifa kuharakisha zoezi la kuondoa miili 8 ya wahamiaji haramu kutoka Ethiopia iliyohifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tanga Bombo kwa zaidi ya miezi miwili na nusu iliyopita baada ya wakala aliyekuwa akiwasafirisha katika bahari ya hindi kutoka nchi jirani ya Kenya kisha kuingia nchini kinyume cha sheria chombo chake kukumbwa na dhoruba.

Akizungumza jijini Tanga kuhusu mustakabali wa miili hiyo naibu kamishna wa uhamiaji ambaye pia ni afisa uhamiaji mkoa wa Tanga Ally Dadi amesema wamewasiliana na ubalozi wa Ethiopia ambao wameomba ifanyike tathmini ya gharama zilizotumika kisha kuwasilishwa katika mamlaka husika ili iweze kusafirishwa lakini hadi sasa zaidi ya miezi miwili na nusu imepita kwa sababu hawana mamlaka ya kuizika miili ya wageni bila kufuata taratibu za kidiplomasia.

Katika zoezi la kukabiliana na uingiaji wa wahamiaji haramu kutoka Ethiopia na Somalia kamanda wa polisi mkoani Tanga kamishna msaidizi mwandamizi jeshi la polisi Edward Bukombe amesema vyombo vya ulinzi na usalama katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari  hadi Desemba mwaka jana vimefanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu zaidi ya 689 kiwango ambacho ni kikubwa ikilinganishwa na idadi ya mwaka 2017 walikuwa 413.

Kuhusu biashara za magendo ambapo mkoa wa Tanga unadaiwa kuwa miongoni mwa mikoa ambayo imekuwa vinara wa kuingiza bidhaa bila kulipiwa ushuru kamanda Bukombe amesema bidhaa mbalimbali kutoka nchi za Brazil na Asia zimekamatwa hasa sukari,mafuta ya kupikia pamoja na bidhaa za magari.