Back to top

Miili ya watu 20 waliofariki wakikanyaga mafuta kwa Mwamposa kuagwa.

03 February 2020
Share

Miili ya watu 20 waliofariki dunia kwenye viwanja vya Majengo Mjini Moshi wakati kukanyaga Mafuta Upako kwenye kongamano la Mtume Boniface Mwamposa inatazamiwa kuagwa leo mara baada ya ndugu kutambua miili ya jamaa zao waliokuwa wamehifadhiwa katika hospitali ya rufaa KCMC na Mawenzi Moshi mkoani Kilimanjaro.

Akizungumza na vyombo vya habari Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Kilimanjaro, Dkt.Anna Mghwira amesema baada ya taratibu kukamilika leo wanatazamia miili ya watu 20 itaagwa uwanja wa Majengo Moshi, Kilimajaro.

Dkt.Mghwira amesema miili yote ya watu waliofariki itafikishwa kwenye uwanja wa majengo leo Februari 03, 2020, ili kuwapa nafasi wananchi kuaga, huku akisisitiza kwamba kwa miili ambayo itakuwa haijapata ndugu zao itarudishwa mochwari mpaka ndugu zao wapatikane, na kusema serikali watahakikisha wanadhibiti aina hii ya mafundisho ambayo yanaonekana kupotosha watu.

Dkt.Mghwira ameendelea kuwasisitiza wananchi kujitokeza katika hospitali ya rufaa KCMC na Mawenzi Moshi mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kutambua ndugu na jamaa zao.

Amesema Mtume Mwamposa anashikiliwa na Jeshi la polisi kwa mahojiano ya kina juu ya mkasa huo uliosababisha watu 20 kufariki, huku akisema kwamba wanashangazwa na kitendo cha Mwamposa kukimbia baada ya tukio hilo, jambo ambalo linawatia mashaka kama alikuwa anatoa huduma ya kweli na yenye tija kwanini alikimbia.

Mkasa huo ulitokea Februari Mosi, 2020, na kupoteza watu 20, hadi sasa miili 14 kati ya 20 ya waliofariki imetambulika, wanawake 15 watoto wa Kike wa nne na mmoja mwanamume, wakati wa kukanyaga Mafuta ya Upako kwenye kongamano la Mtume Boniface Mwamposa kwenye viwanja vya Majengo Mjini Moshi na majeruhi 16 wana endelea na matibabu katika Hospitali za Rufaa za KCMC na Mawenzi.