Back to top

Milioni 480 kujenga bwawa la kunyweshea mifugo Kimambi.

21 September 2021
Share

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.Abdallah Ulega amesema katika bajeti ya mwaka 2021/2022 serikali itajenga bwawa la kunyweshea Mifugo lenye thamani ya Shilingi Milioni 480 katika Kijiji cha Kimambi, Wilayani Liwale, Mkoani Lindi.

Amesema ujenzi wa bwawa hilo utasaidia kutatua changamoto ya maji ambayo inawakabili wafugaji wa maeneo hayo na utasaidia pia kutatua migogoro baina yao na wakulima Wilayani humo.

"Rais Samia Suluhu Hassan anakwenda kuwajengea bwawa lenye thamani ya Shilingi Milioni 480 hapa Kimambi, ujenzi wa bwawa hilo utasaidia kuwaondosha katika migogoro,"-Ulega

Pia Ulega amesisitiza kuwa pesa hizo zipelekwe kufanya kazi iliyopangiwa ya ujenzi wa bwawa la kunyweshea mifugo huku akiwataka viongozi wa Wilaya hiyo kuhakikisha pesa hizo zinatumika vizuri.

Ulega ametoa kauli hiyo katika Wilaya ya Liwale, Mkoani Lindi ikiwa ni sehemu ya kusikiliza kero za wafugaji na wakulima ili kuzitatua.

Ameongeza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amewapa pia Majosho mawili katika Kijiji cha Kimambi na Kijiji cha Luwele.

"Sasa kwa sababu huku mifugo  imekuwa mingi sana, Mimi nakuongezeeni Josho lingine hapa ili mifugo mingi iweze kuogeshwa ,"- Ulega

Kwa upande wake Mbunge wa Liwale, Zuberi Kuchauka ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais wa Awamu ya Sita, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea pesa hizo huku akisema kuwa bwawa hilo likikamilika hawatarajii tena kuona migogoro katika Vijiji vilivyotengwa kwa ajili ya Wafugaji Wilayani humo.