Back to top

Msafara wa Lissu wapigwa mabomu ya machozi Nyamongo.

28 September 2020
Share


Watu kadhaa wamejeruhiwa wilayani Tarime mkoani Mara, baada ya polisi kutumia mabomu ya kutoa machozi kuuzuia msafara wa mgombea Urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA Mheshimiwa TUNDU LISU kuingia eneo la Nyamongo Centre.

Maelfu ya wananchi wa Nyamongo jimbo la Tarime Vijijini waliojitokeza kumlaki Tundu Lissu katika kijiji cha Nyangoto, lakini askari polisi waliuzuia msafara wake kuingia eneo la Nyamongo Centre kuwasalimia wananchi.

Dakika chache baadaye, Mkuu wa Polisi wilaya ya Kipolisi Nyamwaga akawamuru askari wawatawanye wananchi hao kwa mabomu ya kutoa machozi.

Hata hivyo, baada ya moshi wa machozi ya mabomu kutulia, msafara wa kumsindikiza mgombea huyo katika eneo la mkutano uliendelea.
Akihutubia mkutano wa kampeni,Tundu Lissu amelalamikia kitendo hicho cha msafara wake kuzuiwa kwa mabomu.

Akiwa njiani kuelekea mikoa ya Kanda ya Kaskazini, mgombea urais huyo pia alifanya mkutano wa kampeni katika uwanja wa Right to Play mjini Mugumu wilayani Serengeti na kuahidi kuwa kama chama hicho kitapata ridhaa ya wananchi, serikali yake itamaliza migogoro ya mipaka inayoendelea kuibuka baina ya wananchi na mamlaka za hifadhi za taifa baada ya Oktoba 28 mwaka huu.