Back to top

Msongamano wa malori ya makaa ya mawe wasababisha adha kwa wananchi

19 January 2019
Share

Mvua zinazoendelea kunyesha mkoani Ruvuma zimesababisha ubovu wa barabara uliopelekea malori yanayobeba makaa ya mawe kukwama eneo la Amanimakolo wilayani Mbinga na kuleta usumbufu mkubwa kwa wananchi.

Kukwama kwa malori hayo yanayobeba makaa ya mawe  kumesababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi wanaohitaji kwenda hospitali wakitokea Lituhi wilayani Nyasa na Ruanda wilayani Mbinga kunakochimbwa makaa ya mawe kushindwa kupita.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga Bw. Juma Mnwele anasema wamefanikiwa kupunguza msongamano wa malori yaliyokwama na kwamba wana mpango wa kujenga eneo la kuegesha magari ili kuondoa kero hiyo.

Akitembelea eneo hilo hivi karibuni waziri wa ujenzi,uchukuzi na mawasiliano Mhandisi Isaack Kamwelwe amesema kero hiyo ni ya muda mfupi kwa kuwa serikali ina mpango wa kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami.