Back to top

Mtu mmoja akamatwa akiwa na mihuri ya taasisi za umma mkoani Mbeya

02 January 2020
Share

Mtu mmoja ambaye ametambuliwa kwa jina la Abraham Obed anashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Mbeya baada ya kukamatwa akiwa na mihuri 66 ya taasisi mbalimbali za umma ikiwemo mahakama, polisi na benki anayodaiwa kuitumia kutengeneza nyaraka feki na kujipatia kipato.

Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya, kamishna msaidizi mwandamizi wa jeshi la polisi, Ulrich Matei amesema mtuhumiwa amekamatwa akiwa maeneo ya Sokoine jijini Mbeya wakati askari wa jeshi la polisi wakiendelea na misako ya kawaida kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani na utulivu katika kipindi hiki cha mwanzo wa mwaka.

Kamanda Matei amesema baada ya uchunguzi jeshi la polisi limebaini kuwa mtuhumiwa zamani alikuwa mtumishi wa bima na baada ya kuacha kazi ameanza kujihusisha na uhalifu wa kughushi nyaraka kwa ajili ya kujipatia kipato kinyume cha sheria.

Katika hatua nyingine, kamanda Matei amethibitisha kupatikana kwa watoto wawili wa familia moja, ambao waripotiwa kupotea tangu desemba 28 mwaka jana na sasa wamepatikana wakiwa maeneo tofauto mkoani Tabora.