Back to top

Mtu mmoja auawa kwa risasi katika operesheni kuondoa makazi Katavi.

17 January 2019
Share

Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Kashinje Yabona mkazi wa kitongoji cha kamalamamsa katika kijiji cha kapalamsenga wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi ameuawa kwa kupigwa risasi, na wengine watatu wamejeruhiwa na watu wanaodaiwa kuwa askari wa wanyama pori katika operesheni ya kuondoa makazi katika eneo hilo linalodaiwa kuwa ni la mapitio ya wanyama pori.

Kufuatia tukio hilo ambalo limeziacha zaidi ya kaya ishirini bila mahali pa kuishi baada ya nyumba zao kuchomwa moto, na ekari 50 za mahindi kuharibiwa kwa  kile kinachodaiwa sumu , wananchi hao wamemuomba mkuu wa mkoa wa Katavi kufika kuzungumza nao kwani mashamba hayo walipewa kihalali na serikali ya kijiji tangu mwaka 2013.

Kamanda wa polisi mkoa wa Katavi Kamishna msaidizi wa polisi Damas Nyanda amesema kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo inalifanyia kazi tukio hilo na kuongeza kuwa askari walilazimika kufyatua risasi baada ya wananchi kukaidi amri ya kuondoka.