Back to top

Mtumbwi wapinduka Ziwa Tanganyika kumi wafariki.

31 July 2020
Share

Watu kumi wakiwemo watoto wanne wamefariki dunia na wengine zaidi ya mia moja wakiokolewa baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria kutoka kijiji cha Sibwesa kwenda Ikola wilayani Tanganyika mkoani Katavi kupinduka katika ziwa Tanganganyika eneo la kamakara kata ya kalya wilayani uvinza mkoani Kigoma.

Akizungumza kwa njia ya simu Mwenyekiti wa kijiji cha Kashagulu Fred Kalambwe amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo amesema chanzo cha ajali hiyo ni kutokana na mtumbi kupigwa na mawimbi makali yaliyosababisha kugonga mwamba na kisha kuzama huku ukiwa umesheheni mizigo kupita kiasi.

Idadi kamili ya abiria waliokuwa wakisafiri kwa kutumia mtumbwi huo haijafahamika mara moja,na kwamba jitihada za kutafuta miili mingine inayosadikika kupotea ndani ya ziwa Tanganyika inaendelea.

baadhi ya abiria waliokolewa wamepatiwa matibabu katika kituo cha afya cha Kalya na kuendelea na safari kwa kutumia vyombo vingine vya usafiri huku miili ya waliofariki ikitambuliwa na kuchukuliwa na ndugu zao.

Ajali hiyo inakuwa ajali ya pili kutokea ndani ya mwezi mmoja ambapo mnamo June 25 mwaka huu watu tisa walifariki dunia na wengine hamsini na moja kujeruhiwa baada ya boti linalojulikana kwa jina la MV Nzeyimana lilokuwa likifanya safari zake kutoka Sibwesa kwenda Ikola kuzama ndani ya ziwa Tanganyika.