Back to top

Mwili wa Mzee Mkapa kuagwa Kitaifa Julai 28.

24 July 2020
Share

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa ataagwa Kitaifa Jumanne Julai 28 katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam na atazikwa kijijini kwao Lupaso, Masasi mkoani Mtwara Jumatano, Julai 29, 2020.

 “Mwili wa mzee wetu, kiongozi wetu Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu utaanza kuagwa kuanzia Jumapili, Julai 26, 2020 katika Uwanja wa Uhuru ambapo saa 4.00 asubuhi kanisa Katoliki litaongoza ibada na baada ya ibada waombolezaji wataanza kuaga.”

Waziri Mkuu ameyasema hayo  wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Makazi ya Waziri Mkuu Oysterbay jijini Dar es Salaam ambapo amesema zoezi la kuaga mwili litafanyika kwa muda wa siku tatu ambapo wakazi wa jiji la Dar es Salaam pamoja na wananchi kutoka maeneo mengine wataanza kuaga kuanzia Jumapili, Julai 26 hadi Jumanne, Julai 28 siku ambayo mwili utaagwa Kitaifa.

 Waziri Mkuu amesema kwa siku ya Jumanne, Julai 28, 2020 zoezi la kuaga mwili litanyika kuanzia asubuhi hadi saa 6.00 mchana na ifikapo saa 8.00 mchana mwili utasafirishwa kwenda Masasi kwa kupitia uwanja wa Ndege wa Nachingwea na mazishi yatafanyika Jumatano, Julai 29, 2020.

 Mapema, Waziri Mkuu alikwenda nyumbani kwa aliyekuwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa Masaki jijini Dar es Salaam na kutoa pole kwa Mama Anna Mkapa mjane wa marehemu pamoja na familia, kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali.

Kufuatia kifo hicho kilichotokea usiku wa kuamkia leo, Rais Dkt. Magufuli ametangaza siku saba za maombolezo ya Kitaifa kuanzia leo Ijumaa, Julai 24, 2020 na katika kipindi chote cha maombolezo bendera zote zitapepea nusu mlingoti.