Back to top

Ndugu wa Bobi Wine akamatwa na vikosi vya usalama.

20 September 2018
Share


Nduguye mbunge wa upinzani nchini Uganda Bobi Wine, Eddy Yawe na Naibu msemaji wa chama cha Democratic party Waiswa Alex Mufumbiro, wamekamatwa na vikosi vya usalama na kuzuiwa kwenye kituo cha polisi uwanja wa Entebbe huku duru zikieleza kuwa kila mtu wa familia anayewasili uwanja wa Entebbe anakamatwa, licha ya polisi kusema awali kuwa watawaruhusu watu wa familia kumkaribisha Bobi Wine.

Kwa sasa vikosi vya polisi mjini Kampala viko kwenye tahadhari kubwa kabla ya kuwasili kwa mbunge huyo wa Kyadondo East ambaye  anatarajiwa kuwasili Kampala alasiri, leo Alhamisi kutoka nchini Marekani ambapo alikuwa ameenda kupata matibabu baada ya kuripotiwa kuteswa na vikosi vya usalama.

Akiwa nchini Marekani Bobi Wine alifanya mikutano kadhaa na waandishi wa habari, akahojiwa na vituo vingi vya televisheni za kimtaifa ambapo Tangu atangaze kurudi Uganda, makamanda wa polisi mjini Kampala wamekuwa wakifanya mikutano tangu Jumatatu kujiandaa kurudi kwa mbunge huyo.

Kwenye video aliyochapisha kwenye mtandao wa Facebook, Bobi Wine amesema serikali inapanga kuzua ghasia ili kuwalaumu wafuasi wa chama cha People Power ambapo Kulinganga na Bobi, baadhi ya watu wanachapisha shati nyekundu za wafuasi wa People Power na kuwapa majangili wa serikali ili wapate kuzua ghasia ndio waonekane kuwa wao ni wafuasi wake.