Back to top

NEMC yawashukia wafanyabiashara wanao hujumu miundombinu ya SGR.

27 November 2020
Share

Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limewaonya wananchi wanaojihusisha na biashara ya kuuza na kununua vyuma chakavu inayopelekea kuhujumu baadhi ya miundombinu ya serikali ikiwemo reli ya SGR na barabara kuacha mara moja kabla ya kuwachukulia hatua kali za kisheria na kuwaburuza mahakamani.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa NEMC Dkt.Samweli Gwamaka ikiwa ni siku mbili tu jeshi la polisi mkoani Pwani kukamata gari aina ya Fuso lililokuwa na namba za ujajili T-167-DJW likiwa limebeba vyuma chakavu vilivyochanganyika na vyuma vya mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR.

Dkt.Gwamaka amesema NEMC itaendelea kufanya ukaguzi nchi nzima katika maeneo ambayo wafanya biashara wa vyuma chakavu wanafanyia biashara zao lengo likiwa kuwabaini wale wote ambao wanaohujumu miundo mbinu ya serikali na kuendesha biashara ya vyuma chakavu bila kuwa na kibali kutoka NEMC.

Gwamaka ameongeza kuwa kwa sasa gari hilo aina ya fuso lililokuwa limebeba vyuma hivyo chakavu linashikiliwa kwenye kituo cha polisi Mlandizi mkoani Pwani pamoja na watu watatu waliokuwa na gari hilo.