Back to top

Nipigieni simu hata saa nane za usiku kwa askari wanaowaomba rushwa.

16 August 2019
Share

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu amesema Wizara hiyo itaendelea kupunguza adha mbalimbali zinazowakabili Wadau wa Utalii likiwemo suala la polisi wa usalama barabarani kusimamisha magari yenye watalii mara kwa mara.  

Amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau wa utalii nchini imejenga vituo vya ukaguzi wa magari vya utalii ili kupunguza usumbufu kwa watalii barabarani.

Amesema vituo hivyo vitashughulikia masuala ya msingi likiwemo suala madereva wenye watalii kupimwa kilevi.

Amesema mbali na kilevi, Vituo hivyo vitashughulikia vitendo vyote ya uhalifu watakavyofanyiwa watalii.

Aidha, Mhe.Kanyasu amesema lengo la Serikali ni kupunguza kero kwa watalii ili wafikie milioni mbili mwaka 2019.

Mhe.Kanyasu amesema licha ya  kujengwa vituo hivyo vya ukaguzi lakini bado kuna kero ambazo  zinafanyiwa kazi lengo likiwa ni kuboresha sekta ya utalii.

Kwa upande wake, Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Jonathan Shana amewataka wadau wa utalii kufuata sheria lakini akataka kupewa taarifa za polisi wanaowakwaza.

Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Jonathan Shana.

"Nipigieni simu hata saa nane za usiku kwa askari wanawaomba rushwa nishughulike nao" Alisisitiza Shana.

Naye Mkuu wa mkoa wa Arusha Mhe.Mrisho Gambo amesema lengo la Arusha kuanzisha vituo vya ukaguzi magari ni kupunguza kero.

Amesema uwepo wa vituo hivyo vitafanya  mazingira bora kwa  watalii na wafanyabiashara.

Mwenyekiti wa Chama cha Wasafirishaji Watalii (TATO) Wilbard Chambulo amesema ujenzi wa vituo hivyo ni hatua muhimu ya kuwahakikishia watalii usalama wao pindi  wakiwa barabani pamoja na mali zao.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Prof.Adolf Mkenda amesema mkoa wa Arusha ni mfano wa kuigwa kwa mikoa mingine kwa kujenga vituo hivyo ili kupunguza kero kwa watalii.