Back to top

Nyaraka za mradi wa ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Mbarali zayeyuka.

19 October 2018
Share

Nyaraka muhimu za mradi wa ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya zimepotea katika mazingira ya kutatanisha na kusababisha hofu ya kuwepo ubadhirifu wa fedha kwenye mradi huo.
Upotevu wa nyaraka za mradi huo uliosimama  kwa muda kutokana na ukosefu wa fedha, umebainika baada ya serikali kuu kutoa fedha shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuendeleza mradi huo na katika hatua za kutaka kuendelea na ujenzi ndipo ikabainika kuwa nyaraka muhimu hazijulikani zilipo.

Makamu mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mbarali, Mhe.Bahati Salum amesema jitihada za kutafuta nyaraka hizo katika ofisi za wakuu wa idara zimegonga mwamba hali inayoashiria  kuwepo kwa ubadhirifu wa fedha.

Mkuu wa wilaya ya Mbarali, Reuben Mfune amesema baada ya kupata taarifa ya upotevu wa nyaraka hizo, aliunda tume ya kuchunguza suala hilo, lakini hata tume yake hiyo imeshindwa kujua mahali zipo nyaraka za mradi huo na ndipo ameamua kulipeleka suala hilo TAKUKURU akidai kuwa jitihada za kushughulikia suala hilo kiutawala zimeshindikana.