Back to top

Nyuki wvamia shule na kujeruhi mwanafunzi mmoja.

21 March 2019
Share

Taharuki imezuka katika shule ya msingi Kikundi katika manispaa ya Morogoro baada ya nyuki kuvamia ghafla na kumjeruhi vibaya mwanafunzi mmoja wa darasa la kwanza mwenye umri wa miaka 11, Junior Benedict, hali iliyosababisha shughuli za masomo kusitishwa kwa muda na walimu kufunga ofisi wakihofia usalama wao.

Wazazi na walezi wenye wanafunzi katika shule hiyo ya msingi Kikundi wamefika shuleni hapo na kuulaumu uongozi kwa kushindwa kuchukua hatua kuwaondoa nyuki hao waliomshambulia vibaya mwanafunzi huyo na kuvimba zaidi maeneo ya kichwani na usoni.

Mganga Mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro dk ritta lyamuya amekiri hospitali hiyo kumpokea mwanafunzi mmoja ambaye amelazwa wadi namba nne akipatiwa matibabu.

ITV ikamtafuta mwalimu mkuu wa shule hiyo kutoa ufafanuzi wa tukio hilo bila mafanikio lakini Afisa elimu msingi wa manispaa ya Morogoro Abdul Buheti akizungumza kwa njia ya simu akakiri tukio hilo kufikishwa ofisini kwake na tayari wameshalifikisha kwa afisa nyuki ili kuwaondoa nyuki hao na wanafunzi waweze kuendelea na masomo.