Back to top

Ongezeko la mifugo lachangia migogoro na uharibifu wa mazingira Rufiji

15 July 2019
Share

#PICHA_NA_MAKTABA.

 

Ongezeko la mifugo katika vijiji mbalimbali vya wilaya ya Rufiji mkoani Pwani inayochangia kuharibu mazingira na misitu limekuwa kikwazo kwa uhifadhi endelevu wa misitu ya vijiji misitu ambayo kwa miaka ya karibuni imekuwa na mchango mkubwa kwa uchumi na maendeleo ya wananchi.


Mkuu wa wilaya ya Rufiji mkoani Pwani Juma Abdallah Njwayo amesema tatizo la mifugo ikiwemo iliyoingia kutoka bonde la Ihefu ni changamoto namba moja katika wilaya hiyo kwani idadi iliyopo sasa ni kubwa ikilinganishwa na uwezo wa wilaya kupokea ng'ombe elfu hamsini ingawa amesema kwakuwa wafugaji hao ni Watanzania serikali haiwezi kuwafukuza lakini kwa sasa wilaya imekataa kupokea mifugo mipya.


Baadhi ya viongozi wa vijiji vya wilaya ya Rufiji kikiwemo kijiji cha Nyamwage wamesema pamoja na umuhimu wa mifugo kwa maendeleo lakini ongezeko la wafugaji limekuwa likisababisha migogoro baina ya wakulima na wafugaji na hasa mwaka huu ambapo mvua hazikunyesha za kutosha hali inayowafanya baadhi yao kuingiza mifugo na kulisha kwenye mashamba ya wakulima.


Nae Afisa Mtendaji wa kijiji cha Nyamwage Evena Michael amesema kutokana na rasilimali za misitu kijiji hicho kimepata zaidi ya shilingi milioni 100 ambazo zimetumika kujenga ofisi ya mfano ya kijiji na pia kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya jamii ikiwemo ya afya na elimu.