Back to top

Polisi walitambua gari iliyotumika kumteka mfanyabiashara Mo Dewji.

19 October 2018
Share

Mkuu wa jeshi la polisi nchini IGP SIMON SIRRO amesema katika muendelezo wa upepelezi kuhusu kutekwa kwa mfanyabishara maarufu na bilionea Mohamed Dewji  wamefanikiwa kutambua gari iliyotumiwa kumteka mfanyabiashara huyo.

Mohamed Dewji - Mfanyabiashara aliyetekwa Oktoba 11,2018 wakati akielekea kufanya mazoezi katika hoteli Colosseum, Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Kamanda Sirro  amesema gari hilo ambalo muundo wake ni Toyota  Surf  na lenye rangi ya bluu nyeusi, na lenye ufito wa rangi ya shaba kwa chini lilitokea nchi jirani ambayo hakuitaja na kueleza kuwa liliingia nchini Tanzania mnamo  Septemba mosi mwa ka huu ambapo amesisitiza kuwa wanafuatilia kwa kushirikiana na polisi wa kimataifa wa Interpol.

Mkuu wa Jeshi la polisi nchini Tanzania IGP Simon Sirro 

Amesema kufikia sasa hawafahamu iwapo gari hilo, ambalo wamebaini nambari yake ya usajili ni AGX 404 MC, bado lipo Tanzania na akawaomba wananchi kutoa taarifa kwa polisi iwapo wakiliona.

Sirro amesema kwa kutumia kanda za kamera za CCTV wamebaini kwamba gari hilo aina ya Surf baada ya kutoka hoteli ya Colosseum, lilipita barabara za Haile Sellasie, Ally Hassan Mwinyi, Maandazi, Mwai Kibaki na kisha likapotelea kwenye eneo la Mlalakuwa karibu na mzunguko wa Kawe.

Kamanda sirro pia amesema kufikia sasa watu nane bado wanashikiliwa na polisi kuhusiana na kisa cha kutekwa kwa Mohamed dewji huku akitoa wito kwa wafabnyabiashara wenye ukwasi kuhakikisha wanakuwa na ulinzi imara katika utekelezaji wa shughuli zao mbalimbali.