Back to top

Raia nane wa kigeni kutoka nchini Ethiopia wakamatwa.

11 July 2018
Share

Idara ya uhamiaji mkoa wa Dodoma imewakamata raia nane wa kigeni kutoka nchini Ethiopia,Rwanda na uganda kwa makosa ya kutofuata taratibu na sheria za kuingia nchini, huku wahamiaji haramu 64 raia wa Ethiopia waliokamatwa wakiwa kwenye lori mapema mwezi Machi mwaka huu wakihukumiwa kifungo cha mizezi mi tano jela na lori waliokuwa wakisafiria likitaifishwa na Mahakama.

Akizungumza na waandishi wa habari Naibu Kamishna wa Uhamiaji mkoa wa Dodoma Peter Kundy amesema mbali na raia hao wa Ethiopia walioingia nchini bila kufuata taratibu pia wamewakamata raia wawili watanzania kwa makosa ya kutotoa ushirikiano kwa askari wakati wa upekuzi.

Aidha katika hatua nyingine Naibu Kamishna Kundy amesema mbali na misako mbalimbali pamoja na operesheni zinazoendelea za kuwasaka wahamiaji haramu pamoja na raia wa kigeni wanaoingia nchini bila kufuata taratibu ni jukumu la wananchi kutoa ushirikiano kwa idara ya uhamiaji katika kuwafichua watu hao.

ITV imezungumza na baadhi ya wakazi mkoani Dodoma ambapo wamesema vitendo vya kuwaficha wahamiaji haramu au raia wa kigeni nchini bila kufuata taratibu ni kosa ambalo pia linaharibu sifa ya nchi huku wakiziomba mamlaka husika kuongeza kasi ya mapambano.