Back to top

Raia wa Zambia waandamana na kuchoma matairi kwenye forodha ya Tunduma

24 March 2019
Share

Raia wa Zambia wameandamana na kuchoma magurudumu ya magari katika barabara inayounganisha forodha za Tunduma Mkoani Songwe na Nakonde Nchini Zambia.

Raia hao wa Zambia walikuwa wakishinikiza Polisi upande wa Tanzania kuwaachilia huru raia wenzao wa Zambia 15 waliokamatwa na polisi kituo cha Tunduma kwa makosa ya uhalifu mpakani kufuatia operesheni inayofanywa na Kamati ya usalama mpakani.

Vurugu hizo zimedumu kwa takribani saa tatu zikiambatana na urushaji wa mawe kwa magari na Watanzania waliotaka kuvuka upande wa Zambia ambapo katika madai yao walitaka raia 15 waliokamatwa na kamati ya ulinzi forodha ya Tunduma upande wa Tanzania waachiliwe huru.

Raia wa Tanzania wamekosoa vikali msimamo wa waandamanaji wa Zambia na kuwataka viongozi wa pande zote mbili kuweka mikakati shirikishi kuzuia mizozo ya aina hiyo kujirudia.

Viongozi wa Wilaya za Nakonde upande wa Zambia na Momba upande wa Tanzania wamefanikiwa  kukomesha mogoro  huo kwa kuzingatia sheria za forodha na kwa pamoja wameridhia wahalifu hao kutoachiliwa huru badala yake wahamishiwe upande wa Zambia na kushughulikiwa kwa mjibu wa sheria za forodha.

Mzozo huo umekwisha baada ya majadiliano ya kina baina ya kamati za Usalama upande zote mbili.