Back to top

Raia watatu wa Thailand wakamatwa uwanja wa ndege KIA.

12 July 2018
Share

Raia watatu kutoka nchini Thailand wamekamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa kilimanjaro (KIA) kwa kosa la kuingia nchini wakiwa na fedha za kigeni dola za Kimarekani zaidi ya laki moja na themanini sawa na zaidi ya shilingi milioni 40 za kitanzania kwa ajili ya ununuzi wa madini katika jiji la Arusha kinyume na taratibu na sheria za uingizwaji na usafirishaji wa fedha nchini.

Afisa Mfawidhi wa forodha uwanja wa  ndege wa kimataifa Kilimanjaro (KIA) Bw.Lazaro Magovongo amesema abiria hao walikamatwa wakati wa kufanyiwa ukaguzi katika mashine za kukagua mizigo na mabegi ya abiria katika kitengo cha Mamlaka ya Mapato Tanzania( TRA)

Amesema abiria hao baada ya kuhojiwa kwa tuhuma za kukutwa na fedha hizo walisema walikua wanaelekea katika jiji la Arusha kwa ajili kufanya biashara ya madini.


Kwa upande wake Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Kilimanjaro Bw.Msafiri Mbibo amesema jitihada za kunasa fedha hizo zimetokana na mashine ya kisasa ya ukaguzi wa mizigo na mabegi ya abiria iliyowekwa na serikali kwa ajili  ya wasafiri wanaoingia na kutoka katika uwanja huo.

Naye Meneja Msaidizi wa ushuru wa forodha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Kilimanjaro Bw.Godfrey Kitundu amesema watuhumiwa watafikishwa mahakamani na kwamba wakibainika kuwa na makosa watachukuliwa hatua za kisheria ikwemo faini au kifungo.