Back to top

Rais asikitishwa na idadi ya Watanzania waliopoteza maisha,atoa pole.

02 February 2020
Share

Rais Dkt. John Pombe Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa familia za watu 20 waliopoteza maisha wakati wa kongamano la kukanyaga mafuta lililoandaliwa na Mtume Boniface Mwamposa Moshi Mkoani Kilimanjaro, na kwa familia za watu zaidi ya 20 waliopoteza maisha kutokana na madhara ya mvua kubwa zinazonyesha Mkoani Lindi na Mikoa mingine hapa nchini. 


Mhe. Rais ameeleza kusikitishwa na idadi kubwa ya vifo vya Watanzania waliopoteza maisha katika matukio hayo, na amewaombea Marehemu wote wapumzike mahali pema peponi na Majeruhi wote wapone haraka na kurejea katika majukumu yao.

Amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Anna Mghwira, Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Godfrey Zambi na Wakuu wa Mikoa wengine ambao Mikoa yao imepatwa na madhara ya watu kupoteza maisha kutokana na madhara ya mvua, kufikisha salamu zake za pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na vifo hivyo.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa Watanzania wote kuchukua tahadhali katika matukio yote yenye viashiria vya hatari ikiwemo mikusanyiko mikubwa ya watu na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha na amevitaka Vyombo vya Ulinzi na Usalama kuhakikisha vinasimamia ipasavyo tahadhali za kiusalama.