Back to top

Rais Dkt.Magufuli aahidi kutoa shilingi Bilioni 1.5 MOI

10 September 2019
Share

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 10 Septemba, 2019 amemjulia hali Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam Mhashamu Yuda Thaddaeus Ruwa’ichi ambaye amelazwa katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) Jijini Dar es Salaam.

Baba Askofu Mkuu Ruwa’ichi alipatwa na ugonjwa wa kiharusi juzi huko Moshi Mkoani Kilimanjaro ambako alianza kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kilimanjaro (KCMC), na kisha kupelekwa MOI ambako amefanyiwa upasuaji wa kichwa na anaendelea na matibabu.

Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu wa MOI Prof. Joseph Kahamba amesema baada ya kufanyiwa upasuaji huo hali ya Baba Askofu Ruwa’ichi imeanza kuimarika.
Mhe. Rais Magufuli pamoja na Madaktari na Wauguzi wa MOI
wamemuombea Baba Askofu Ruwa’ichi ili apone haraka na kuendelea na majukumu yake ya kila siku.

Akiwa katika wodi hiyo ya wagonjwa mahututi, Mhe. Rais Magufuli amewajulia hali wagonjwa wengine waliofanyiwa upasuaji wa kichwa na kuelezea kufurahishwa na maendeleo makubwa yaliyopatikana katika taasisi ya MOI ambayo sasa inatoa matibabu ya upasuaji mkubwa ambayo hayakuwa yanapatikana hapa nchini.

Prof. Kahamba amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa Serikali kufanya uwekezaji mkubwa katika taasisi ya MOI katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita ikiwemo kukamilisha jengo, kuongeza vitanda vyote vinavyohitajika 2 Ikulu Mawasiliano, 10 Septemba, 2019

katika vyumba vya upasuaji na chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), kununua vifaa vipya vya uchunguzi kama vile MRI, CT-Scan, Digital x-ray, Ultrasound na sasa mipango inaendelea kununua kifaa kiitwacho Endovascular Neurosuite ambacho kinagharimu shilingi Bilioni 7.5 hali iliyoiwezesha MOI kufikia viwango vya kimataifa.

Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Madaktari na Wauguzi wa MOI kwa kazi kubwa wanayoifanya na ameahidi kutoa shilingi Bilioni 1.5 kwa taasisi hiyo kwa ajili ya kununulia vipandikizi kwa ajili ya wagonjwa wanaopatiwa
matibabu baada ya kuvunjika.

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Respecious Boniface amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kutoa fedha hizo na kumhakikisha kuwa zitasaidia katika matibabu ya Watanzania wengi.

Akiwa njiani kurejea Ikulu, Mhe. Rais Magufuli ametembelea Kituo cha Polisi cha Selander Bridge na kuzungumza na Askari wa Kituo hicho ambapo ameagiza WP 4160 Beatrice Kayuni Mlanzi kupandishwa cheo kutoka Koplo na kuwa Sajenti baada ya kuonesha utimilifu katika kazi.