Back to top

Rais Magufuli akutana na Madaktari bingwa kutoka Israel, Marekani.

08 November 2018
Share

Uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Tano kufungua Ubalozi wa Tanzania nchini Israel umeanza kuzaa matunda baada ya timu ya madaktari na wataalamu wa matibabu ya moyo 30 kutoka nchini Israel kuja hapa nchini kwa ajili ya kuokoa maisha ya watoto 51 wanaopatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Jijini Dar es Salaam.

Timu ya Madaktari na wataalamu hao wakiwemo 2 kutoka Marekani na Canada wanatoka shirika la Save a Child’s Heart la Israel wamekutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli,  Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Prof. Mohamed Janabi amesema kati ya watoto 51 wanaopatiwa matibabu katika kampeni hii 10 watafanyiwa upasuaji wa kufungua kifua na 20 watafanyiwa upasuaji kwa kutumia tundu dogo.

Kiongozi wa timu ya Madaktari hao na Mkurugenzi Mtendaji wa Save a Child’s Heart Bw. Simon Fisher na Mkuu wa Kitengo cha upasuaji wa moyo wa shirika hilo Prof. Sasson Lior wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa ushirikiano mkubwa ambao timu hiyo inapata kutoka Serikali ya Tanzania na wameahidi kuwa taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na Tanzania kuokoa maisha ya watoto.

Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amemuandikia barua ya shukrani Mhe. Netanyahu na kuikabidhi kwa Balozi wa Israel hapa nchini Mhe. Noah Gal Gendler ambapo pamoja na kushukuru kwa msaada wa matibabu pia amemshukuru kwa ushirikiano katika sekta nyingine.