Back to top

Rais Magufuli alipa jina Daraja la Ubungo kuwa Daraja la Kijazi.

24 February 2021
Share

Rais wa Tanzania Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli amelizindua Daraja la juu la Ubungo na kulipa jina la Daraja la Juu la Kijazi ikiwa ni katika kumuenzi aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali aliyefariki dunia Februari 17, 2021.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi ya siku tatu jijini Dar es Salaam Mhe.Magufuli amesema ameamua kuliita daraja hilo jina la BALOZI KIJAZI kutokana na mchango wake mkubwa aliofanya kwa kiasi kikubwa katika kusimamia mafanikio ya utekelezaji wa miradi mbalimbali iliyokamilika na kuwataka Watanzania kulitunza daraja hilo.

Mhe.Magufuli amesema Ujenzi wa mradi huo wa daraja la juu Ubungo ambalo limejengwa kwa ngazi tatu umesaidia kupunguza adha ya Msongamano wa vyombo vya moto na ajali katika Makutano ya ubungo ambayo awali ilikua ni shida kwa wakazi wa jiji hilo katika eneo hilo ambalo kwa siku linapita magari zaidi ya elfu sitini na nane mia nane na thelathini na tisa( 68839).

Sambamba na uzinduzi wa daraja hilo la juu Mheshimiwa Rais Magufuli amezindua Kituo kipya cha kimataifa cha mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi cha kilichopo eneo la Mbezi Luis jijini Dar es Salaam kinachotarajiwa kuanza kutoa huduma siku ya kesho Alhamisi ya Februari 25, 2021.

Mhe.Magufuli Kesho anatarajiwa kuendelea na ziara ya kikazi kwa kuweka jiwe la msingi katika soko la kisasa Kisutu pamoja na kuzindua jengo la jitegemee mnazi mmoja na kuhitimisha ziara hiyo Siku ya ijumaa atakapozindua majengo ya chuo cha polisi na kiwanda cha sare za Polisi kurasini.