Back to top

Rais Magufuli amfuta kazi mtumishi wa serikali aliyechana Quran.

11 February 2020
Share

Rais Dkt.John Magufuli amemfukuza kazi mtumishi wa Halmashauri ya Kilosa mkoani Morogoro Daniel Maleki kwa kitendo cha kuchana kitabu cha Quran na kusema kwamba hawezi kukaa na wafanyakazi wapumbavu katika serikali yake.

Amempongeza Waziri wa TAMISEMI Mh.Selemani Jafo kwa hatua za mwanzo alizokuwa alizochukua.

"Juzi nilikuwa namsikia Mhe Jafo, mtu mmoja kule Kilosa nafikiri alichana kitabu kitakatifu, nashukuru umechukua hatua ya kumsimamisha kazi, lakini mimi namfukuza kazi moja kwa moja.. hatuwezi kukaa na watu wapumbavu, atajua mwenyewe atakapo yatafuta maisha".Rais Magufuli.

Baada ya tukio hilo Februari 07, 2020 Waziri wa TAMISEMI Selemani Jafo aliliagiza jeshi la polisi mkoani Morogoro kuhakikisha  linamkamata kijana huyo na kumuhoji, na kwamba tayari wanamshikilia kijana huyo aliyeonekana kwenye video fupi akichana na kuitemea mate Quran Tukufu.

Kwa mujibu wa Kamanda Mutafungwa alisema baada ya upelelezi kufanyika tayari kijana huyo amekwishafikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kilosa na kusomewa mashtaka ya kuudhi na kukashfu dini.

Video hiyo fupi ilisambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii, ikimuonesha kijana huyo ambaye anadaiwa kuwa ni Mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kitengo cha Biashara, akichana kitabu hicho cha dini, Juzuu Amma ambayo ni sehemu ya Quran Tukufu.