Back to top

Rais Magufuli amlilia Moi, atuma salamu za pole kwa Rais Kenyatta.

04 February 2020
Share

Rais wa Tanzania Mhe. Dkt.John Pombe Magufuli amemtumia salamu za pole Rais Uhuru Kenyatta pamoja na Wakenya kwa ujumla katika kipindi hiki kigumu kwa taifa hilo kutokana na Kifo cha Rais Mstaafu wa Kenya Daniel Arap Moi aliyefariki dunia leo Nairobi Hospital alikokuwa akipatiwa matibabu tangu.

Rais Dkt.Magufuli ametoa salamu hizo za pole kupitia mtandao wake wa Twitter ambapo ameandika "Kwa niaba ya Serikali na Watanzania nakupa pole Mhe.Rais Uhuru Kenyatta na Wakenya wote kwa kuondokewa na Rais Mstaafu Daniel Toroitich arap Moi"-Rais Magufuli. 

Amesema Watanzania wataendelea kumkumbuka Daniel Arap Moi kwa uongozi wake mahiri na juhudi za kuimarisha mahusiano mazuri kati ya Tanzania na Kenya"Watanzania tutamkumbuka kwa uongozi wake mahiri, jitihada za kuimarisha uhusiano wetu na Kenya na kufufua Jumuiya ya Afrika Mashariki"-Rais Magufuli.

Aidha taarifa za Kifo cha Rais Mstaafu wa Kenya Daniel Arap Moi kilitangazwa hii leo na Rais Uhuru Kenyataa wa Kenya, ambapo Runinga ya taifa ya Kenya (KBC), pamoja na vyombo binafsi vya Capital FM, Citizen TV na NTV viliweza kuripoti taarifa hiyo ya msiba asubuhi ya leo Jumanne, Februari 4.  

Marehemu Daniel Arap Moi alizaliwa 1924 na amewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini, ikiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani (1964), Makamu wa Rais (1967 - 1978), Agosti 22, 1978 akawa Rais wa Kenya hadi Disemba 30, 2002, ambapo amefariki akiwa na umri wa miaka 95.