Back to top

Rais Magufuli amtumbua Mwijage amteua Kakunda kuwa waziri wa Viwanda

10 November 2018
Share

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli leo tarehe 10 Novemba, 2018 amefanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri kwa kuteua Mawaziri wawili na Naibu Mawaziri wanne. 

Kwanza, Mhe. Rais Magufuli amemteua Mhe. Japhet Ngailonga Hasunga kuwa Waziri wa Kilimo.

Kabla ya uteuzi huo Mhe. Hasunga alikuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, na anachukua nafasi ya Mhe. Dkt. Charles John Tizeba ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Kabla ya uteuzi huo Mhe. Hasunga alikuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, na anachukua nafasi ya Mhe. Dkt. Charles John Tizeba ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Pili, Mhe. Rais Magufuli amemteua Mhe.Joseph George Kakunda kuwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Kabla ya uteuzi huo Mhe. Kakunda alikuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), na anachukua nafasi ya Mhe. Charles John Mwijage ambaye uteuzi wake umetenguliwa. 

Tatu, Mhe. Rais Magufuli amemteua Mhe. Constantine John Kanyasu kuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii. Mhe. Kanyasu anachukua nafasi ya Mhe. Hasunga ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo.

Nne, Mhe. Rais Magufuli amemteua Mhe. Dkt. Mary Machuche Mwanjelwa kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. 

Kabla ya uteuzi huo Dkt. Mwanjelwa alikuwa Naibu Waziri wa Kilimo.

Tano, Mhe. Rais Magufuli amemteua Mhe. Mwita Mwikwabe Waitara kuwa Naibu Waziri wa TAMISEMI. Mhe. Waitara anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Mhe. Kakunda ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Sita, Mhe. Rais Magufuli amemteua Mhe. Innocent Lugha Bashungwa kuwa Naibu Waziri wa Kilimo. Mhe. Bashungwa anachukua nafasi ya Mhe. Dkt. Mwanjelwa ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Uteuzi wa viongozi hawa umeanza leo tarehe 10 Novemba, 2018 na wateule wote wataapishwa Jumatatu tarehe 12 Novemba, 2018 saa 3:00 asubuhi, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho Mama Anna Margareth Abdallah na kuivunja bodi hiyo kuanzia leo tarehe 10 Novemba, 2018.