Back to top

Rais Magufuli kuwa mgeni rasmi katika sherehe za Mei Mosi Mbeya.

24 March 2019
Share

Rais Dkt.John Pombe Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe za maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani maarufu kama Mei Mosi ambayo mwaka huu yatafanyika kitaifa Mkoani Mbeya.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Bwana Albert Chalamila ametoa taarifa hiyo wakati wa kikao cha pamoja baina ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mbeya na viongozi wa kitaifa wa Shirikisho la Vyama vya wafanyakazi nchini, kwa ajili ya kuanza maandalizi ya sherehe hizo.

Kutokana na ujio wa Rais Dkt.John Pombe Magufuli mkoani Mbeya kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe kuwa Rais, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,  Bwana Albert Chalamila amewataka wananchi na wakazi wa mkoa huo kuitumia siku hiyo kama fursa nzuri na kubwa ya kiuchumi, fursa ya kujenga uhusiano mzuri na fursa pekee ya kuendeleza Mkoa wa Mbeya.

Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania, Bwana Tumain Nyamhokya amewataka viongozi wa wilaya zote za Mkoa wa Mbeya kuungana katika maandalizi ya maadhimisho hayo ya Mei Mosi, pamoja na kushiriki kwa ukamilifu.