Back to top

Rais Magufuli leo amefanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri

08 January 2019
Share

Rais  Dkt. John Pombe Magufuli  amefanya uteuzi wa nafasi mbalimbali za uongozi uliotangazwa na Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Ikulu Jijini Dar es Salaam ambapo  amemteua Mhe. Anjellah Kairuki kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji ambapo kabla ya uteuzi huo Mhe. Kairuki alikuwa Waziri wa Madini.

Katika mabadiliko hayo aliyekuwa naibu waziri wa madini  Mhe. Doto Biteko ameteuliwa kuwa kuwa Waziri wa Madini ambapo sasa wizara hiyo  itakuwa na naibu Waziri mmoja ambaye Mhe. Stanslaus Nyongo huku Mhandisi Joseph Nyamuhanga akiteuliwa kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Aidha  Dkt. Zainabu Chaula ameteuliwa  kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto  anayeshughulikia afya huku Elius Mwakalinga akiteuliwa kuwa Katibu Mkuu Ujenzi akitokea  Wakala wa majengo ambapo alikuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala huo.

Mhe. Rais Magufuli amemteua Bi. Dorothy Mwaluko kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uwekezaji),Dkt. Dorothy Gwajima kuwa Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI (Afya),Dkt. Francis K. Michael kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mpoki Ulisubisya ameteuliwa  kuwa Balozi na kituo chake cha kazi kitatangazwa hapo baadaaye.

Prof. Faustin Kamuzora ameteuliwa  kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera akichukua nafasi ya  Bw. Athumani Diwani Msuya ambaye ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Uapisho wa viongozi hao utafanyika  januari 9 mwaka huu Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameifuta nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi. Nafasi hiyo ilikuwa inashikiliwa Bi. Immaculate Ngwalle ambaye amestaafu.

Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Magufuli amefanya uamuzi wa kufungua Ubalozi mpya wa Tanzania nchini Cuba. Balozi wa Tanzania nchini Cuba atateuliwa baadaye.