Back to top

Rais Magufuli:Serikali inaendelea kuwahimiza wakimbizi kurejea makwao

06 February 2019
Share

Rais Dkt. John Pombe Magufuli amesema pamoja na dhamira njema ya kuwapa hifadhi wakimbizi na kuwapa uraia baadhi ya wakimbizi, Serikali inaendelea kuwahimiza kurejea makwao wakimbizi ambao katika nchi zao machafuko yamekwisha ili wakaungane na familia, ndugu, jamaa na kujenga nchi zao.

Amesema hayo leo ikulu jijiniDar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) Mhe. Filippo Grandi.

Rais Magufuli amesema amefurahi kuwa UNHCR itaendelea kushirikiana na Tanzania pamoja na kuonyesha utayari wa kusaidia gharama za kuhudumia wakimbizi pamoja na jamii katika maeneo wanayoishi wakimbizi maana tangu miaka 10 iliyopita UNHCR imekuwa ikiahidi kutoa fedha za kusaidia wakimbizi lakini haitekelezi ahadi zake.

Kwa upande wake Mhe. Grandi amemshukuru Mhe. Rais Magufuli na Serikali yake kwa kuendelea kuwapokea na kuwapa hifadhi wakimbizi kutoka nchi zenye matatizo mbalimbali na ameomba radhi kufuatia Serikali ya Tanzania kukamata makontena yaliyoingizwa nchini yakiwa na nguo zinazofanana na sare za jeshi na kubainisha kuwa jambo hilo halitajirudia.