Back to top

Rugemarila akabidhi nakala ya barua kwa mwalikishi wa TAKUKURU

30 January 2020
Share

Mfanyabiashara, James Rugemarila ameieleza  Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa tarehe 24 mwezi huu alikutana na mwakilishi wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) alipokuwa ametembelea gerezani na kumkabidhi nakala ya barua aliyoiandika kwenda kwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania jinsi benki ya Standard Chartered Hong Kong walivyokwepa kodi.

Kauli hiyo imekuja baada ya Wakili wa TAKUKURU, Maghela Ndimbo kuiambia mahakama kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi katika shauri hilo haujakamilika.

Bwana.Rugemarila amesema ndani ya barua hiyo ameeleza ni jinsi gani Benki ya Standard Chartered Hong Kong walivyokuwa wakikwepa kodi ya ushuru wa forodha kwa hiyo hadi sasa hajapata mrejesho, hivyo akaiomba mahakama kesi itakapotajwa tena upande wa mashitaka waje na majibu.

Pia ameeleza kuwa wanaotakiwa kushtakiwa ni Benki ya Standard Chartered Hong Kong.

Aidha amesema anashangazwa kuona washtakiwa wengine wanao ongezwa katika kesi hiyo, hivyo upelelezi hautakamilika kama watakuwa wanaongezwa.

Baada ya kusikia hoja hiyo, Hakimu Huruma Shaidi ameiahirisha hadi tarehe 13 mwezi ujao itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.