Back to top

Serikali kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika nchini Juni 13.

12 June 2018
Share

Serikali imepanga kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika nchini mnamo Juni 13 mwaka huu badala ya Juni 16 kama ilivyo kawaida kwa sababu tarehe husika itaingiliana na ratiba zingine.
 
Tamko hilo limetolewa leo jijini Arusha na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika pamoja na kufungua mafunzo ya Waandishi wa Habari za watoto yaliyoandaliwa na shirika la Plan International.
 
Dkt. Ndugulile amesema kuwa Serikali inalinda haki na maendeleo ya watoto ndio maana imeanzisha Idara, Sera na kutengengeneza Sheria zinazomlinda mtoto hivyo maadhimisho hayo yana umuhimu kufanyika kila mwaka.

“Maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika kilele chake ni Juni 16, 2018 lakini kwa mwaka huu tutayafanya siku ya kesho Juni 13 ambayo kitaifa tunayaadhimisha mkoani Arusha,” alisema Dkt. Ndugulile.

Dkt. Ndugulile ameongeza kuwa haki moja wapo ya mtoto ni kuishi hivyo ili kuokoa vifo vya watoto, Serikali imeboresha huduma za afya kwa kutoa chanjo za watoto hao pamoja na kuhakikisha wakina mama wanajifungulia katika vituo vya afya.

Aidha, Dkt. Ndugulile ametoa takwimu za ukatili wa kijinsia za Januari hadi Disemba mwaka 2017 kuwa zimefikia 41,000 ambapo kati ya hizo 13,457 ni za ukatili dhidi ya watoto,
 
Ili kudhibiti matukio hayo, Dkt. Ndugulile amefafanua kuwa Serikali imeanzisha Mahakama za Watoto ambapo mashauri yanayohusiana na watoto yanasikilizwa kwa faragha, imeanzisha mahabusu za watoto ili kuwaweka tofauti na watu wazima pamoja na kuweka namba ya simu ambayo ni 116 kwa ajili ya kutoa taarifa ya ukatili wa kijinsia ili hatua stahiki zichukuliwe.

Vile vile Serikali imekuja na mpango mkakati wa kudhibiti ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto utakaoisha 2022 ambapo kati ya mipango hiyo, imeanzisha kituo kimoja (One Stop Centre) ambacho kitajumuisha huduma za kipolisi, ushauri nasaha pamoja na huduma za kimatibabu kwa waliofanyiwa ukatili wa kijinsia.

Aidha, Dkt. Ndugulile ametoa rai kwa wananchi kutomaliza kesi za ukatili wa watoto kifamilia badala yake kuzifikisha katika vyombo vya kisheria ili hatua za kisheria zichukuliwe kukomesha tabia hizo - Dkt. Ndugulile.

Kwa upande mwingine Dkt.Ndugulile amewakumbusha wanahabari kuacha kusambaza picha au kumtambulisha mtoto ambaye amedhalilishwa kijinsia kwa kuwa ni kosa kisheria.