Back to top

Serikali kuajiri Walimu wapya 6,000 Shule za Msingi, Sekondari Juni 20

09 April 2021
Share

Serikali kupitia Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mh.David Silinde amesema wanatarajia  kuajiri Walimu wapya 6,000 wa Shule za Msingi na Sekondari ifikapo Juni 2021 ili kujaza nafasi zilizoachwa na Walimu waliofariki ama kustaafu kazi.

Akijibu swali bungeni juu ya hatua zinazochukuliwa na serikali katika kumaliza upungufu wa walimu hasa vijijini Naibu Waziri TAMISEMI Mhe.Silinde amesema Katika kukabiliana na changamoto ya uhaba wa walimu katika Shule za Msingi na Sekondari kuanzia Disemba 2015 hadi Septemba 2020, Serikali imeajiri walimu 10,666 wa Shule za Msingi na Walimu 7,515 wa Shule za Sekondari na kuwapanga kwenye maeneo yenye uhitaji mkubwa. 

Aidha, Amesema serikali kupitia Ofisi za Wakuu wa Mikoa imekuwa ikifanya uhamisho wa ndani kwa kuwahamisha walimu waliozidi hasa kwenye maeneo ya mijini na kuwapanga kwenye Shule zenye uhaba mkubwa wa walimu ambazo nyingi zipo maeneo ya vijijini na kwamba  Serikali itaendelea kuajiri na kuwapanga walimu kwenye Shule za Msingi na Sekondari hasa zenye mahitaji makubwa kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.