Back to top

Serikali kudhibiti Ukimwi kwa asilimia 75 ifikapo mwaka 2023.

01 December 2018
Share

Serikali imezindua Mkakati wa Nne wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi 2018/19 - 2022/23 unaotarajia kupunguza maambukizi mapya ya Virusi Vya UKIMWI kwa asilimia sabini na tano  ifikapo mwaka 2020 na asilimia themanini na tano ifikapo mwaka 2023.

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amezindua mkakati huo leo kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika kitaifa jijini Dodoma na kusema matayarisho yake yamezingatia matokeo ya mapitio ya Mkakati wa Tatu wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI 2013/14 - 2017/18.

Amesema matokeo mengine yanayotarajiwa kufikiwa kutokana na mkakati huo ni kupungua kwa maambukizi mapya ya Virusi Vya UKIMWI miongoni mwa watoto kwa chini ya asilimia mitano ifikapo mwaka 2023 na chini ya asilimia mbili ifikapo mwaka 2030.

Amesema mbali na matokeo hayo pia mkakati huo utawezesha kupungua kwa vifo vinavyohusiana na Ukimwi kwa asilimia hamsini ifikapo mwaka 2020 na asilimia sabini ifikapo mwaka 2023 na kupunguza unyanyapaa na ubaguzi ifikapo 2023 na kuelekea kutokomeza kabisa ifikapo mwaka 2030.

Hata hivyo, amesema mkakati huo umewianisha na kupanga programu mbalimbali zinazosaidia mwitikio wa Taifa zikiwemo afua zinazotekelezwa kupitia mpango wa dharura wa Rais wa Marekani wa Ukimwi.

Kuhusu kampeni ya Furaha Yangu aliyoizindua Julai mwaka huu, amesema wananchi laki mbili mia moja na kumi na wanne walijitokeza kupima Virusi Vya Ukimwi na kuitaka mikoa na wilaya kuifanya kampeni hiyo kuwa endelevu.