Back to top

Serikali kuongeza wataalamu wa afya-Majaliwa

21 June 2018
Share

WAZIRI MKUU Mh. Kassim Majaliwa amesema Serikaliitaongeza idadi ya wataalamu wa afya nchini watakaodahiliwa katika vyuo vya afya vya Serikali na binafsi katika programu za Uuguzi na Ukunga, Sayansi Shirikishi za Afya na wahudumu Afya ya Jamii.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Juni 21, 2018) wakati akizindua majengo ya Taasisi ya Elimu ya Afya Mvumi, yaliyojengwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Dunia wa Kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria.

Amesema Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli, itaendelea kushirikiana na wadau wote kuboresha vyuo vya mafunzo ya afya kwa kufanya upanuzi, ujenzi wa majengo na ukarabati.

Waziri Mkuu amesema ukarabati na upanuzi utafanyika katika vyuo vya uuguzi vya Nachingwea, Kibondo, Kagemu, Kondoa, Same na Kiomboi na vyuo vya Mafunzo ya Maafisa Afya vya Bombo (Tanga), Mpwapwa na Ngudu (Mwanza) na Chuo cha Maafisa Tabibu cha Kibaha na Chuo cha Maabara Singida.

Amesema lengo la Serikali ni kuongeza idadi ya wataalamu wa fani mbalimbali wenye uadilifu na weledi wa kustahili pamoja na  kusimamia ubora wa mafunzo ya kada za afya zisizo katika kiwango cha shahada. 

Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali itaongezaidadi ya udahili wa wanafunzi watakaosomea utaalamu wa kibingwa katika fani mbalimbali na kuajiri watumishi wa kada za afya katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini kwa kuzingatia maeneo yenye uhaba mkubwa wa watumishi hususan maeneo ya vijijini.

Amesema Serikali itaendelea itasimamiana kuratibu uandaaji wa wataalamu wa sekta mbalimbali ikiwemo ya afya kutoka vyuoni ili waendelee kuwa nguzo muhimu ya utoaji huduma za afya kwa wananchi. 

Pia,Waziri Mkuu amewasihi wakufunzi wote nchini watekeleze majukumu yao kwa weledi na Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itaendelea kuhakikisha uwepo wa mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia. 

"Vilevile, nitumie hadhara hii kutoa rai kwa wanafunzi wote nchini wasome kwa bidii na kuhakikisha wanahitimu vyema masomo yao ili waweze kutimiza malengo yao binafsi sambamba na kuleta tija na ufanisi kwa Taifa letu muda wote na popote pale watakapokuwa wakitekeleza majukumu yao,".

Awali, Mkurugenzi wa Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii (CSSC), Bw. Peter Maduki alisema mradi huo ambao ulisimamiwa na CSSC ulianza Aprili 2015 na ulitarajiwa kukamilika Mei 2016. "Kutokana na changamoto mbalimbali mradi ulikamilika Machi 2018,".

Alisema mradi huo ambao umegharimu sh. bilioni 5.2 kati yake sh. bilioni 4.4 zilitumika katika upanuzi, ukarabati wa majengo na ujenzi wa majengo mapya ya kulala wanafunzi mawili, jengo la utawala na sh. milioni 864.4 zilitumika kununulia vifaa vya kufundishia.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bibi Ummy Mwalimu, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt.Binilith Mahenge, Mwakilishi wa Global Fund, Bi. Martha Setembo, Mkurugenzi wa Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii Bw. Peter Maduki na Mbunge wa Mtera Bw.  Livingstone Lusinde na Viongozi wa Dini.