
Serikali ipo mbioni kutunga sheria maalum kwa ajili ya kilimo ili kulinda maeneo yote yanayofaa kwa kilimo katika azma yake ya kukuza sekta ya kilimo nchini.
"Katika kulinda maeneo yanayofaa kwa kilimo na kupunguza migogoro ya matumizi ya Ardhi nchini, serikali kupitia wizara ya kilimo tunaendelea na hatua za utungwaji wa sheria ya kilimo"-Mavunde
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Kilimo Mh.Anthony Mavunde, wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Ihusi-Bariadi, Mkoani Simiyu katika mkutano wa hadhara wakati kamati ya Mawaziri 8 wa kisekta wanaoshughulikia migogoro ya Ardhi ya Vijiji 975 walipofika katika eneo hilo.
"Kwakuwa dhamira yetu kubwa ni kuhakikisha tunakuza sekta hii ya kilimo kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030, hatua hii lazima iende sambamba na kuyatambua maeneo ya kilimo na kuyalinda kisheria. Asema Mavunde.
