Back to top

Tani 1,388 za Mahindi zaokolewa kushambuliwa na Viwavijeshi Iringa

23 June 2018
Share

Halmashauri ya wilaya ya Iringa imefanikiwa kuokoa tani 1388 za Mahindi baada ya kufanikiwa kuzima tishio la Viwavijeshi vamizi waliokuwa wameanza kushambuli jumla ya hekta 697 katika halmashauri hiyo.

Taarifa hiyo imetolewa na afisa kilimo ofisi ya mkuu wa mkoa wa Iringa Revocatus Rwegoshola katika kijiji cha Muwimbi wilayani Iringa na kuwataka wakulima kuendelea kutoa ushirikiano kwa serikali kwa kutoa taarifa mapema mara wanapogundua tofauti kwenye mazao yao.

Leomacha Mavika ni kutoka ofisi ya rais TAMISEMI idara ya kusimamia sekta za uchumi na uzalishaji anasema kutokana na wakulima wa zao la mahindi kuzalisha kwa wingi kwa msimu pili mfululizo serikali imeziagiza halmashauri zote zinazozalisha zao la Mahindi kukusanya takwimu ili kujua ziada ya chakula kinachohitajika kuuzwa.

Kwenye sherehe za mavuno katika kijiji cha Muwimbi kata ya Lumuli halmashauri ya Iringa imesaini mkataba na shirika lisilo la kiserikali la One Acre Fund kufanya kazi kwa pamoja katika sekta ya kilimo ambapo shirika hilo linalotoa mikopo ya pembejeo pamoja na huduma za ugani kwa wakulima litaendelea kufanya shughuli hizo kwa lengo la kusaidia wakulima kuinua uzalishaji.