Back to top

TBS yakamata shehena ya Mabati yaliyotengenezwa chini ya kiwango Mbeya

10 March 2019
Share

Shirika la viwango nchini (TBS) limekamata na kusitisha uuzwaji wa shehena ya mabati ya kisasa zaidi ya 2000 yenye migongo mipana maarufu kwa jina la msauzi yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 60 kwa madai kuwa yametengenezwa chini ya kiwango na hayafai kwa matumizi.

Maofisa wa shirika la viwango nchini Tanzania, TBS, wamefanya ukaguzi wa kushtukiza katika maghala ya mawakala wa makampuni matatu yenye viwanda vya kutengeneza mabati nchini yaliyopo jijini Mbeya ambako wamefanikiwa kukamata shehena ya mabati ambayo yanadaiwa kutengenezwa chini ya kiwango na kusitisha uuzwaji mabati hayo ambayo sasa yanasubiri taratibu zikamilike ili yateketezwe.

Licha ya mabati hayo kudaiwa kuwa chini ya kiwango bado yamebandikwa nembo ya ubora ya TBS hali ambayo ikamlazimu mkaguzi wa viwango kutoka TBS, Baraka Mbajije kutoa ufafanuzi huku akidai kuwa hilo ni kosa la matumizi mabaya ya nembo ya ubora ambalo pia itawabidi wazalishaji wa mabati hayo kuwajibika.

Baadhi ya mawakala wa makampuni ya kuzalisha mabati hayo wamegoma kuzungumzia suala hilo kwa madai kuwa wao sio wasemaji wa makampuni yao, huku afisa uhusiano wa shirika la viwango nchini, TBS, Roida Andusamile akiwataka wananchi kususia bidhaa zisizokuwa na ubora ili kuepuka hasara wanayoweza kuipata.