Back to top

Tetemeko laikumba mikoa mitatu laua mmoja na kuharibu mali .

21 March 2019
Share

Tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa kipimo cha richta 5.1 limeyakumba maeneo ya jirani na ziwa Rukwa ikiwemo mikoa ya Katavi,Mbeya na Songwe na kusababisha kifo cha mtu mmoja mkoani Songwe na uharibifu wa mali kwenye mikoa hiyo.

Kwa mujibu wa Mjiolojia mwandamizi kutoka taasisi ya jiolojia iliyo chini ya Wizara ya madini Gabriel Mbogoni amesema tetemeko hilo limetokea majira ya saa sita na robo mchana katika maeneo hayo yaliyo jirani na ziwa Rukwa na kudumu kwa sekunde kadhaa.

Katika mkoa wa Songwe Kamanda wa polisi wa mkoa George Kyando amesema mkazi wa kijiji cha Iyula kata ya Iyula aliyefahamika kwa jina la Mwanji Elias Mtega amefariki dunia baada ya kuangukiwa na nyumba yake iliyoshindwa kuhimili kishindo cha tetemeko hilo.

Mkoani Mbeya tetemeko hilo limesababisha uharibifu wa majengo ambapo mpaka sasa nyumba nne zimebomoka huku jengo la ghorofa tano la shirika la nyumba la taifa likipata nyufa na kuifanya moja kati ya benki ambayo imepanga katika jengo hilo kusitisha shughuli zake mpaka litakapohakikiwa ubora wake.

Napo mkoani Rukwa tetemeko hilo limesababisha taharuki ambapo katika manispaa ya Sumbawanga wakazi wa manispaa hiyo walionekana wakikimbia huku na huku kujiokoa, hasa wafanyakazi waliokuwa kwenye majumba ya ghorofa mjini humo na mpaka sasa hakuna madhara yaliyojitokeza kwa watu ama mali zao.

Wakazi wa mikoa hiyo wamesema waliona ardhi ikitisika na wao kulazimika kukimbia kwa ajili ya kujinusuru na tetemeko hilo.