Back to top

Tunduru yaanza kutumia waganga wa tiba asili kuibua wagonjwa wa TB

22 February 2020
Share

Baadhi ya wananchi katika halmashauri ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, wameipongeza serikali kupitia kitengo cha kifua kikuu na ukoma kutoka hospitali ya wilaya ya Tunduru, kwa kuanza kuwatumia waganga wa tiba asili waliosajiliwa kuibua wagonjwa wa kifua kikuu na kuwafikisha hospitali kwa ajili ya kupata matibabu stahiki.
 
Miongoni mwa vituo vya waganga wa tiba asili maarufu kwa jina ya “Vilinge” ambavyo ITV imevitembelea ni pamoja na kilinge cha babu Manjenje katika kijiji cha Namasalau-Mdingula Tunduru ambaye alipata mafunzo ya kuwaibua wagonjwa wa kifua kikuu pindi wanapowabaini.
 
Nao baadhi ya wananchi wameipongeza serikali  wilayani humo kwa kuwatumia waganga wa tiba asili kuwaibua wagonjwa wa kifua kikuu huku wakitoa wito pia kuwatembelea mara kwa mara.

Mratibu wa kifua kikuu na ukoma kutoka hospitali ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Daktari Mkasange Kihongole anasema tayari waganga wa tiba asili zaidi ya 40 wameshapata mafunzo namna ya kuwaibua wagonjwa wenye maambukizi ya kifua kikuu na kwamba hadi sasa hakuna mti shamba uliobainika unaweza kutibu ugonjwa huo.