Back to top

Uboreshaji daftari la wapiga kura Mwanza laingia dosari.

13 August 2019
Share

Zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura katika baadhi ya vituo vya uandikishaji vya jiji la Mwanza, limeanza kwa kuingia dosari kufuatia baadhi ya mashine za mfumo wa kusajili wapiga kura kwa kutumia alama za vidole ( BVR), kubainika kuwa na hitilafu hatua ambayo imesababisha usumbufu kwa wananchi waliojitokeza kwenye zoezi hilo.

Katika kituo cha ofisi ya afisa mtendaji wa kata ya Isamilo kilichopo eneo la Nera jijini Mwanza, baadhi ya wananchi wamelalamikia ubovu wa mashine hizo ambazo zimesababisha kukaa muda mrefu kituoni, huku mafundi wanaotakiwa kutengeneza mashine hizo wakidaiwa kuchukua muda mrefu kushughulikia tatizo hilo.

Awali akizindua zoezi hilo katika kituo cha polisi eneo la wazi kata ya Kiseke manispaa ya Ilemela, mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongela amewaagiza watumishi wa tume ya taifa ya uchaguzi kuongeza kasi ya kuandikisha wananchi ili zoezi hilo katika awamu ya kwanza liwe limekamilika ifikapo Agosti 19 mwaka huu.

Baadhi ya wakazi wa mtaa wa PPF Kiseke katika jimbo la uchaguzi la Ilemela waliodamkia kwenye zoezi hilo wamewashauri wenzao kutumia fursa hiyo adhimu kurekebisha taarifa zao ili wapate sifa za kupiga kura katika uchaguzi mkuu ujao.

Tume ya taifa ya uchaguzi imetenga jumla ya vituo 2,178 vya uandikishaji wapiga kura kwenye kata 191 na majimbo 9 ya uchaguzi katika halmashauri nane za mkoa wa Mwanza. 

Zoezi hilo la uboreshaji wa daftri la kudumu la wapiga kura katika mkoa huu litafanyika kwa awamu mbili, awamu ya kwanza itahusisha wilaya za Ukerewe, Magu, Misungwi, Sengerema, Ilemela na Nyamagana, ambapo awamu ya pili itahusisha wilaya moja tu ya kwimba kuanzia Agosti 26 hadi Septemba Mosi mwaka huu.