Back to top

Ugonjwa wa “Kwangua vocha” unavyowatesa wananchi Butiama

03 December 2019
Share

Wakazi wa kijiji cha Ryamisanga wilaya ya Butiama mkoa  wa Mara wamekumbwa na ugonjwa  wa kuwashwa na kuota upele  katika maeneo mbalimbali ya miili yao hususani kwenye mikono, miguu na  tumboni  huku wakiubatiza jina la  ugonjwa wa kwangua vocha kutokana na kujikuna mara kwa mara hali inayopelekea upele huo kutunga usaha na wakati mwingine kutokwa na damu wakati wanapojikuna 

Ukisikia kwangua vocha unaweza ukapata picha ni kitendo cha kukwangua vocha  ya kuongeza muda wa maongezi  kwenye simu,lakini kwa wakazi wa kijiji cha Ryamisenga wao kwangua vocha ni ugonjwa ambao umeondoa furaha na tabasamu kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa tangu ugonjwa huo udaiwe kuingina ndani ya kijiji hicho ambao umesababisha kuharibu ngozi za miili yao.

ITV imepata taarifa za uwepo wa ugonjwa huo ndani ya basi ,baada ya mwanamke mmoja kuingia ndani ya basi lililokuwa likisafiri kutoka Musoma mjini kuelekea Serengeti akiwa amejaa upele mwili mzima pamoja na mtoto wake ,ndipo ITV ilipomdadisi mwanamke huyo na kudai  anaugua ugonjwa wa kwangua vocha na kwamba ni ugonjwa ambao umevamia kijiji chao.

Baada ya taarifa hiyo ITV ikafunga safari kuelekea katika kijiji hicho na  kisha  kushuhudia watoto, wazee, vijana na wanawake  wakiwa na upele na kujikuna kila wakati huku watoto wakionekana kuathirika zaidi ambapo wamesema ugonjwa hupo umewatesa kwa muda mrefu kila wakienda hospitali wanachomwa sindano na kupewa dawa za kupaka lakini hawaponi huku wakishangaa ni ugonjwa wa aina gani huo ambao pia unasababisha watoto kupinda vidole na miguu huku watu wazima wakidai kuoza sehemu za siri za miili yao

Kwa upande wake mganga mfawidhi  wa hospitali ya kijiji hicho amesema ugonjwa huo upo na kudai unasababishwa na kijiji hicho kukosa maji jambo linalopelekea wananchi kutokuoga vizuri na kwamba ugonjwa huo pia unaambukizwa  na wanyama kwani baadhi ya wakazi wa kijiji hicho wanalala na mifugo ndani.