Back to top

Uhamiaji Rukwa yawasaka wahamiaji ziwa Tanganyika bila ya Boti.

20 August 2018
Share

Wahamiaji walowezi zaidi ya 5,600 wamefikiwa hadi sasa mkoani Rukwa, katika zoezi linalotekelezwa na idara ya uhamiaji mkoani humo, huku zoezi likikwamishwa na ukosefu wa vitendea kazi, ikiwa ni pamoja na vyombo vya usafiri hasa boti kwenye ziwa Tanganyika, ambako kuna vijiji zaidi ya hamsini katika mwambao wa ziwa hilo, na baadhi yake havifikiki kabisa kwa barabara.
 
Kaimu afisa uhamiaji wa mkoa wa Rukwa naibu kamishna Elizeus Mushongi, akiongea mjini Sumbawanga amesema maafisa uhamiaji wamekuwa wakitekeleza zoezi hilo, ikiwa ni pamoja na kuwasaka wahamiaji haramu katika mazingira magumu mno, kwani baadhi ya vijiji vilivyoko kwenye mwambao wa ziwa Tanganyika katika wilaya za Kalambo na Nkasi, havifikiki kwa njia ya barabara ni lazima kuingia ndani ya ziwa hilo, ambalo linafanya mkoa wa Rukwa upakane na nchi za Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na Zambia.
 
Kwa upande wake afisa wa hati za kusafiria mkoani Rukwa mrakibu msaidizi wa uhamiaji Sharifa Mangosongo, akizungumzia juu ya upatikanaji wa hati hizo za kusafiria za kieletroniki, amesema sasa hivi hali imeboreshwa mno na kwamba hati hizo zinapatikana mkoani humu, na kwa kutumia muda mfupi kuliko ilivyokuwa hapo awali.