Back to top

Ushirikiano wa TRA na wafanyabiashara waendelea kuimarika.

24 May 2018
Share

Mamlaka ya Mapato  nchini  TRA  imesema  mahusiano  na  ushirikiano   kati  ya  mamlaka  na  wafanyabiashara  umeendelea   kuimarika  na  kuleta  tija  kwa  wananchi   na  taifa  kwa  hatua  ambayo  mkurugenzi wa  elimu  ya mlipakodi  Bw. Richard  Kayombo  amesema  umeanza  kurahisisha  ulipaji   wa  Kodi  na  pia  kupunguza  gharama za  ukusanyaji.

Akizungumza  na  walipakodi   mkoani   Arusha  Bw.   Kayombo  amesema  baada  ya  wafanyabishara  kuanza  kuelewa  umuhimu  wa  kulipa  kodi   na  pia  kuona  matokeo  ya kodi   zao   asilimia  kubwa   sasa  wanalipa   kwa  hiyari  na  wanatoa ushirikiano  mkubwa  ukiwemo   wa  kufichua   wachache  wanaoendelea  kukwepa kodi   na  mbinu  wanazotumia.

Kuhusu   hatua  iliyofikiwa  kudhibiti   ukwepaji  wa  kodi  kwa  bidhaa  zinazotoka  nje  Bw. Kayombo  amesema  pia  tatizo  hilo  linaendelea  kupungua   kutokana  na  kuimarishwa  kwa ushirikiano   na wenzao   wa  nchi jirani  na ameendelea  kuwaomba  wafanyabishara  kutumia  fursa  za  soko  la pamoja  na  Jumuiya  ya Afrika  Mashariki  kufanya  biashara halali  ili  kuepukana  na  hasara  zisizo   za  lazima  kwani  biashara za  magendo  kwa  sasa  hazina  nafasi.

Baadhi  ya wafanyabishara  wamekiri  kuboreka  kwa  mahusiano   miongoni  mwao  na TRA  na wameitaka  mamlaka  hiyo   kuendelea  kuyaboresha  hasa  wakati  huu  ambao  hali  ni  ngumu   kwani  hata wao   wanafurahia  kulipa kodi    na  wanaona  matokeo  yake.