Back to top

Utiaji saini mkataba wa Amani wakwama

21 July 2018
Share

Kutiwa saini kwa mkataba wa awali wa amani kati ya Rais SALVA KIIR wa Sudan Kusini na mpinzani wake RIEK MACHAR kumeahirishwa, baada ya viongozi hao kushindwa kueWANA kuhusu namna ya kugawana madaraka.
Mkataba huo ulitarajiwa kutiwa saini jijini Khartoum nchini Sudan na baadaye makubaliano rasmi kutiwa saini tarehe 26 mwezi huu.

Taarifa zinasema serikali ya Sudan Kusini ndiyo iliyokataa kusaini mkataba huo baada ya Rais SALVA KIIR, kuonekana kutokuwa tayari kuwa na makamu watano wa rais.

Pande hasimu za Sudan Kusini zimeafiki kugawana madaraka kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa na pande hizo ambapo kwa mujibu wake kiongozi wa waasi nchini humo, RIEK MACHAR atarejeshwa katika wadhifa wa Makamu wa Rais.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan, AL DIERDIRY AHMED alisema hivi karibuni kuwa imeafikiwa kwamba kutakuwepo makamu wanne wa rais; yaani makamu wawili wa rais waliopo hivi sasa pamoja na RIEK MACHAR, na nafasi ya nne ya makamu wa rais atapangiwa mwanamama kutoka kambi ya upinzani.

Pande hizo mbili zilifikia makubaliano hayo katika juhudi za kuhitimisha vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyozuka mwaka 2013 baada ya hitilafu za kisiasa kati ya Rais SALVA KIIR na aliyekuwa makamu wake, MACHAR na kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe.