Back to top

Vijana wa kike 300 waomba kuongezewa mitaji wajikwamue kiuchumi Rukwa

10 July 2018
Share

Vijana wa kike zaidi ya 300 katika kata ya Chala wilayani Nkasi Rukwa, waliopata mafunzo ya ufundi stadi baada ya kukatisha masomo yao, wameiomba serikali iwawekee mazingira mazuri ya kupata mitaji, ili waongeze uwezo wa kutengeneza bidhaa nyingi zaidi na kujikwamua kiuchumi kuliko ilivyo hivi sasa.
 
Vijana hao wa kike ambao miongoni mwao walikatisha masomo yao kwa kupata mimba, wakizungumza katika kijiji cha Londokazi wilayani Nkasi, wamesema wamepata mafunzo ya kutengeneza bidhaa mbalimbali za ujasiriamali yaliyotolewa na taasisi ya elimu ya watu wazima, kwa kushirikiana na taasisi ya Common Wealth of Learning COL ya nchini Canada, na kwamba tatizo kubwa wanalokabiliana nalo ni kukosa mitaji, na hivyo kujikuta wakitengeneza bidhaa chache mno.

Kwa upande wake mratibu wa mradi wa kuzuia mimba na ndoa za utotoni unaoendeshwa na taasisi ya elimu ya watu wazima, kwenye wilaya za Nkasi na Kalambo mkoani Rukwa Bi. Leonia Kasamia, ameziomba halmashauri za wilaya za Kalambo na Nkasi kuweka mazingira mazuri, ili kuwaongezea nguvu mabinti hao ambao maisha yao yaliharibika baada ya kukatisha masomo yao wajikwamue kimaisha.