Back to top

Vilio vyatawala miili ya wanafunzi 10 ikiagwa.

18 September 2020
Share

Miili ya wanafunzi 10 waliokufa kwa ajali ya moto uliounguza bweni la wavulana katika Shule ya Msingi Byamungu iliyopo wilayani Kyerwa mkoani Kagera imeagwa leo na kukabidhiwa kwa wanafamilia tayari kwa mazishi.

Zoezi hilo limefanyika katika viwanja vya shule hiyo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi  Dkt.Bashiru Ally aliyekuja kwa niaba ya Rais Magufuli.

Akiongea katika hadhara hiyo Dkt. Bashiru amewapa pole wafiwa na jamii nzima iliyoguswa na msiba huo ambapo amewasihi wafiwa kuwa na subira katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo huku akiitaka serikali pamoja na vyombo vya usalama kuendelea kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha moto huo.

Dkt.Bashiru ameitaka serikali na viongozi wa mkoa wa Kagera kusimamia maagizo aliyoyatoa Rais Magufuli alipokuwa Bukoba na kuwataka wamiliki wa shule kuendelea kutoa ushirikiano pale watakapohitajika.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti amesema kuwa serikali imekuwa bega kwa bega na Wanakyerwa na hasa wafiwa kwa kuhakikisha marehemu wanahifadhiwa vizuri na majeruhi wanatibiwa ambapo amesema kuwa tayari zimeundwa kamati za uchunguzi kwenye shule zote za bweni mkoani humo kwa ajili ya kuangalia miundombinu.

Gaguti ameongeza kuwa kwenye msiba huu serikali imegharamia mazishi ya wanafunzi waliofariki ikiwemo usafirishaji wa mili na matibabu ya majeruhi waliopo hospitalini.

Usiku wa kuamkia Septemba 14 mwaka huu ilitokea ajali ya moto katika Shule ya Msingi Byamungu ambapo bweni la wavulana kwenye shule hiyo liliuungua na kusababisha vifo vya watoto 10 na wengine kujeruhiwa.