Back to top

Viongozi wawili wa UVCCM wilayani Tarime wanashikiliwa na Polisi.

19 July 2018
Share

Viongozi wawili wa Umoja wa vijana wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Tarime mkoani Mara,wanashiliwa na Jeshi la Polisi Kanda maalum ya Tarime na Rorya kwa tuhuma za kumfanyia fujo Waziri wa Maliasili na Utalii Mh Hamis Kigwangalla,kutoa lugha chafu dhidi ya serikali ya awamu ya tano,kisha kula njama kwa kuweka mawe katika barabara aliyokuwa akipita kiongozi huyo na msafara wake.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Tarime na Rorya,Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi nchini Henry Mwaibambe,amesema viongozi hao wanashikiliwa wakati jeshi hilo likifanya uchunguzi ili kukamilisha taratibu za kuwafikisha mahakamani watuhumiwa hao.

Kwa sababu hiyo kamanda huyo wa polisi kanda hiyo amesema baada ya uchunguzi huo kukamilika jarada la watumiwa hao litafikishwa kwa mwanasheria wa serikali kwa hatua zaidi.

Akiwa wilayani Tarime Waziri wa Maliasili na Utalii kukagua maeneo ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti yanayodaiwa kuvamiwa na baadhi ya watu wakiwemo kiongozi mmoja wa CCM wilaya ya Tarime kwa kujenga na kuendesha shughuli nyingine za jamii,viongozi hao wa umoja wa vijana wa CCM wanadaiwa kuikashifu serikali kuwa inaendeshwa kidikiteta huku wakishabikia uwekaji wa mawe na vizuizi katika barabara iliyotumiwa na msafara huo.