Back to top

Wadau wachangia shilingi milioni 150 kukabiliana na Corona.

04 May 2020
Share

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama amepokea msaada wa hundi tatu zenye thamani ya sh. milioni 150 zilizotolewa na kampuni tatu zinazozalisha nguzo za umeme nchini kwa ajili ya kusaidia mapambano dhidi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona (COVID- 19).

Waziri amepokea michango hiyo kwa niaba ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa leo tarehe 4 Mei, 2020 katika Ofisi ya Waziri Mkuu Mlimwa, Jijini Dodoma. Michango hiyo imetolewa na kampuni Mufindi Woodpoles Plant and Timber Ltd, Qwihaya General Enterprises Co Ltd na Poles (T) Ltd ambapo kila kampuni imetoa sh. milioni 50.

Akizungumza wakati wa kupokea michango hiyo Waziri Mhagama aliwapongeza viongozi wa kampuni hizo kwa kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuhakikisha inapambana na janga la ugonjwa wa COVID-19.

Pia, Waziri Mhagama alitumia fursa hiyo kuwasihi wakandarasi wengine pamoja na Watanzania kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kujitolea kwa hali na mali ili kuwezesha katika kukabiliana na janga hilo.