Wafanyabiashara Mkoani Arusha wamelalamikia matatizo yanayoendelea kujitokeza katika matumizi mfumo wa ukusanyaji wa Kodi kwa kutumia mashine za EFD ambazo wamesema licha ya kuonekana kuwa na tija kwa upande wa serikali kwa upande wao zinawaumiza na kuwasababishia uhasama na serikali usio wa lazima.
Wakizungumza katika kikao cha kujadili matatizo hayo wafanyabiashara hao wamesema kadiri siku zinavyokwenda changamoto zilizoko kwenye mashine hizo zinaongezeka na wanapouliza hawapati majibu sahihi na wana hofu kuwa huenda kuna tatizo ambalo ufumbuzi wake haujulikani ama zimehujumiwa na wajanja wachache.
Wakizungumzia malalamiko hayo baadhi ya mawakala wanaosimamia mashine hizo pamoja na kukiri kuwa kuna matatizo wamesema asilimia kubwa yako nje ya uwezo wao kwani yanatokana na mfumo.
Meneja wa TRA Mkoa wa Arusha Bw Faustine Mdessa amesema pamoja na kuwepo kwa changamoto alizodai kuwa ni za kawaida amesema pia baadhi ya wafanyabiashara bado wanakwepa kodi kwa makusudi.
Akizungumza baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Arusha Bw Gabriel Dakharo amesema inavyoonekana lipo tatizo la msingi ambalo ufumbuzi wake ni kila upande kutimiza wajibu wake.
Pamoja na mfumo wa ukusanyaji wa kodi kwa kutumia mashine za EFD kuonyesha mafanikio bado yapo malalamiko yanayotolewa na baadhi ya wafanyabiashara ambayo kundi la wafanyabiashara wanadai kuwa kuna wajanja wanazi hujumu huku mawakala wakidai kuwa ni ujanja wa baadhi ya watu wanaotaka kuendelea kukwepa kodi.